Ujumbe wa Marekani wawasili Damascus kwa mazungumzo
20 Desemba 2024Wanadiplomasia hao watakutana na wawakilishi wa kundi la Hayat Tahrir al-Sham (HTS) ambalo hadi hivi sasa Marekani bado imeliorodhesha kama kundi la kigaidi. Wizara ya mambo ya Nje ya Marekani imesema wajumbe hao pia watazungumza na wanaharakati wa demokrasia nchini Syria, wawakilishi wa makundi ya wachache pamoja na mashirika ya kiraia.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Matthew Miller, amesema wajumbe hao watazungumza na Wasyria kujua matarajio yao kuhusu mustakabali wa nchi yao na jinsi Marekani inavyoweza kuwasaidia.
Wajumbe hao ni pamoja na mwakilishi anayesimamia maswala yanayohusu mateka wa Marekani ambaye amekuwa akitafuta njia angalau za kupata fununu kuhusu Wamarekani waliopotea akiwemo mwandishi wa Habari Austin Tice, aliyetekwa nyara nchini Syria mnamo Agosti mwaka 2012.
Soma Pia: Viongozi wa EU watahadharisha kuhusu mustakabali wa Syria
Ujumbe huo wa kidiplomasia ni wa kwanza, rasmi kutoka Marekani uliokwenda mjini Damascus tangu vilipoanza vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe mnamo mwaka 2011 na ambavyo vimemalizwa na mashambulizi ya ghafla ya mwezi huu wa Desemba yalimwondoa madarakani mtawala wa muda mrefu wa Syria Bashar al-Assad.
Safari hiyo ya ujumbe wa Marekani imefanyika wiki moja tu baada ya Waziri wa Mambo ya Nje Antony Blinken, kusema kwamba Marekani imekuwa ikiwasiliana moja kwa moja na kundi la HTS, alipozuru nchi jirani na Syria.
Katika mazungumzo huko nchini Jordan, mataifa yenye nguvu ya Magharibi na yale ya Kiarabu pamoja na Uturuki yalisisitiza juu ya kuundwa serikali ya Syria ambayo ni jumuishi, isiyoegemea madhehebu yoyote ya dini kwa kuziwakilisha dini zote na pia serikali ambayo itaheshimu haki za Wasyria wote bila kujali nasaba zao tofauti tofauti.
Wito huo uliungwa mkono katika mazungumzo ya Cairo siku ya Alhamisi na nchi za Uturuki na Iran, ambazo ziliunga mkono pande tofauti katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.
Rais wa Iran Masoud Pezeshkian, ambaye nchi yake ilimuunga mkono Bashar al- Assad, alitoa wito wa kushirikishwa kwa makundi yote nchini Syria katika serikali ijayo pamoja na kuheshimiwa kwa imani na dini tofauti tofauti.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, ambaye aliunga mkono upande uliokuwa unampinga Bashar al-Assad, alitoa wito wa maridhiano na kurejeshwa kwa uadilifu na umoja nchini Syria.
Soma Pia: Umoja wa Mataifa watoa wito wa uchaguzi huru Syria
Ziara ya wanadiplomasia hao wa Marekani huko Damascus haitazamiwi kuleta matokeo ya haraka juu ya kufunguliwa tena ubalozi wa Marekani. Kulingana na maafisa wa Marekani, ni kwamba maamuzi juu ya kidiplomasia ya kuitambua serikali ya Syria yatatangazwa pale mamlaka mpya ya Syria itakapoweka wazi nia na mikakati yake.
Vyanzo: AFP/AP